browser icon
You are using an insecure version of your web browser. Please update your browser!
Using an outdated browser makes your computer unsafe. For a safer, faster, more enjoyable user experience, please update your browser today or try a newer browser.

SIRI YA MAFANIKIO YA USAFI WA MAZINGIRA

Posted by on January 6, 2014

 

HALIMASHAURI YA MANISPAA YA MOSHI

UTANGULIZI

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa Halmashauri saba (7) zinazounda Mkoa wa Kilimanjaro. Mji wa Moshi ulianzishwa mwaka 1892, ukahamishiwa mahali ulipo sasa toka Kolila Old Moshi (Moshi Vijijini) mwaka 1911 kutokana na gari moshi kushindwa kupanda eneo hilo. Mwaka 1926 ulipewa hadhi ya Mji mdogo na mwaka 1956 ukapewa hadhi ya  Halmashauri. Ulipewa hadhi ya  kuwa Manispaa mwaka 1988 hadi sasa.

002

ENEO LA MANISPAA.

Manispaa ya moshi imezungukwa na  Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kwa upande wa kusini, mashariki na kasikazini, upande wa magharibi imepakana na wilaya ya Hai.Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ina eneo la kilometa za mraba 58. Halmashauri inatarajia  kuongeza eneo lake hadi kufikia  kilometa za mraba 142  ili kuweza kuwa jiji ifikapo mwaka 2015 litakaloendeshwa kwa utawala bora.

Untitled

IDADI YA WAKAZI.

Mji wa moshi unakadiriwa ulikuwa na idadi ya watu 8,048 mwaka 1948 idadi hiyo ilifikia watu 13,762 mwaka 1957. Mwaka1969 ilikuwa 26,969. Mwaka wa 1988 idadi hiyo iliongezeka nakufikia watu 96,838 hiki ndicho kipindi mji wa moshi ulipewa hadhi ya kuwa manispaa. Mwaka 2002 idadi ya watu ilikuwa144,336. Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa mujibu wa  Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ina jumla ya wakazi  184, 292 na ongezeko kwa mwaka ni  asilimia 2.8, idadi hiyo inajumuisha wanawake 95,118 na wanaume 89, 174. Idadi hii haijumuishi idadi ya watu 76,000 hadi 85,000   wanaoingia Manispaa kila siku asubuhi kwa ajili ya biashara na shughuli mbalimbali  za kiuchumi na kurudi majumbani mwao katika Wilaya za Hai, Rombo, Same, Mwanga na Halmashauri ya Wilaya  ya Moshi majira ya jioni.

DIRA YA HALMASHAURI

Ni kuwa mfano bora kwa kutoa huduma bora katika Nyanja zote za kijamii, kutoa ushauri wa kitaalamu na kujenga uwezo wa wadau kwa lengo la kukuza uchumi na kupunguza umasikini ifikapo mwaka 2025 pamoja na kufikia malengo ya millenia (MDGs)

UTAWALA

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ina Tarafa 2 ambazo ni Moshi Mashariki na Moshi Magharibi, kata 21 Mitaa 60 Kaya 41,345 zenye wastani wa watu 5.

Katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kuna Jimbo moja la uchaguzi.Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ina jumla ya madiwani 29.

MATARAJIO YA MANISPAA

Kuboresha huduma za jamii zinazotolewazo kwa kushirikisha wananchi/wadau wake katika  kupanga na kutekeleza mipango yao ya maendeleo itakayokuwa endelevu. Katika miaka (10) ijayo kuanzia mwaka 2005 Manispaa inatarajia kuwa Jiji litakaloendeshwa kwa misingi ya Utawala Bora.  Pia Manispaa inatarajia kuboresha huduma za jamii kwa kushirikisha wananchi/wadau wake.

USAFI NA MAZINGIRA

2.0. TATIZO LILILOKUWEPO KABLA YA UDHIBITI BORA WA TAKA NGUMU

Kati ya miaka ya 1990 na 2000, idadi ya watu katika Manispaa ya Moshi iliongezeka kwa kasi kubwa ikiwa ni pamoja na wakazi wa kutwa kutoka  Wilaya za jirani za Hai, Rombo, Mwanga na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi  wanaokuja mjini kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kurudi katika wilaya zao jioni.

Mji  wa Moshi umekuwa kutokana na mji mdogo uliokuwa na wakazi 8048 mwaka 1948 na kufikia  wakazi 13,762 mwaka 1957.  Mwaka 1969 kulikuwa na wakazi 26,969 ambapo waliongezeka kufikia wakazi 52,223 mwaka 1978 na wakazi 96,838 mwaka 1988.  Kutokana na sensa ya idadi ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2002, Manispaa ya Moshi ilikuwa na wakazi 143,799 wakiwemo wanawake 73,121, na wanaume 70,678.

Ongezeko hili lilisababisha kuwepo kwa makazi holela, kuongezeka kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na hivyo kuongezeka kwa uzalishaji taka ngumu mara dufu na kufikia kiasi cha tani 145 mwaka 2002 kutoka tani 100 mwaka 2000 hadi kufikia tani  220 kwa sasa.

Kwa wakati huo uondoshajiwa taka ngumu haukuweza kwenda sambamba na uzalishaji kutokana na kukosa miundo mbinu madhubuti ya kukusanya, kusafirisha na utupaji salama.  Magari manne yaliyokuwepo yalikuwa na umri mkubwa na machakavu.Magari hayo yalitolewa kwa msaada wa serikali ya Japan mwaka 1987 na kwa kipindi hicho yaliweza kuhudumia takribani tani 100 zilizozalishwa.

Uwezo wa Idara ya Afya kwa wakati huo kugharimia jukumu la usafi wa mji lilikuwa kubwa kwa kuwa uendeshaji wa shughuli zote ulikuwa unategemea fedha za ruzuku, kwani dhana ya uchangiaji huduma ya uzoaji taka ilikuwa mpya na ngeni.  Sheria zilizokuwepo zilikuwa haziendi na wakati na pia dhana ya ushiriki na ushirikishwaji wadau ilikuwa haijaanza kutekelezwa.Kwa wakati hou Halmashauri ilikuwa inatumia sheria ya Tanganyika 1947 sura 101.

 

MALENGO

Ni kutunza na kuinua kiwango cha usafi wa mazingira na hatimaye kupunguza kuenea kwa magonjwa yatokanayo na mazingira yaliochafuliwa na kuharibiwa.Lengo mahusisi ni kutuo elimu ya kuchambua na kutenganisha taka ngumu (separation at source)ili tupate taka rejea ziweze kutumika kama mali ghafi viwandani. Vile vile tuweze kupata taka zinazooza ili ziweze kutumika kutengeneza bio gas.

SHUGHULI ZILIZOTEKEZWA

 1. Kutoa elimu kwa ajili ya kupunguza magonjwa ya kuambukiza, vifo na madhara mbalimbali kwa wananchi hasa watoto yanayotokana na mazingira duni.
 2. Kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kudumisha afya na usafi wa mazingira.
 3. Kupanua ushirikishwaji wa jamii na hivyo kuwapa madaraka zaidi katika kushugulikia masuala ya afya na usafi wa mazingira.
 4. Kuwezesha jamii kubadili tabia na mazingira wanayoishi kwa kufanya usafi na kupanda miti.
 5.  Kuongeza uwajibikaji kwa watendaji na wadau mbalimbali katika suala zima la usafi wa mzingira
 6. Kuimarisha Usimamizi wa Sheria ndogo ya Usafi wa Mazingira 2006

Manispaa ya Moshi inayo sheria ndogo ya Usafi wa Mazingira ya mwaka 2006 ambayo imefanyiwa marekebisho Aprili 2012 ikisaidiana na sheria ndogo ya Ada na Ushuru ya 2006, zinatosheleza kusimamia shughuli zote za usafi wa mji. Sheria hizi zinasimamiwa kwa karibu sana na kusababisha usafi wa mazingira kuonekana na kila mkazi, mgeni. n.k.

 1. Idara kuratibu vyema shughuli za usafishaji na mazingira.

Idara ya usafi na mazingira inafanya shughuli mbalimbali za kuwezesha mji kuwa katika hali ya usafi na mazingira kupendeza. Shuhuli hizi zinajumuisha;

 • Ukusanyaji wa taka ngumu kwa kutumia magari ya kawaida, uhifadhi kwa kutumia maghuba pamoja na usafishaji taka ngumu jalalani ambapo zina ifadhiwa kwa njia salama.
 • Uzaliji wa miche ya miti mbalimbali ya matunda, kivuli na maua katika kitalu cha manispaa.
 • Kuhamasisha uanzishwaji na uendelezaji wa vitalu vya miche pamoja Na upandaji miti katika kata 21 za manispaa
 • Ufagiaji wa barabara za kati ya mji, kituo kikuu cha mabasi na shanty town ambapo utekelezaji ni waasilimia 100%

 • Kufweka nyasi pembezoni mwabarabara, maeneo ya wazi na kuokota taka zinazo tupwa ovyo ambapo utekelezaji ni 100% pamoja na usafisha mifereji ya maji ya mvua

 

MIKAKATI YA UTEKELEZAJI

 Ushirikishwaji:

 • Suala la usafi wa mazingira katika Manispaa ya Moshi ni suala la wakazi wote.  Ukianzia kwenye menejimenti, tuna utaratibu wa kutumia timu na vipaumbele katika suala la usafi.

Usafi wa mazingira ni suala la kwanza la kipaumbele kila siku na mtendaji mkuu anahakikisha kuwa mafuta, vifaa vyote kwa siku vipo kwenye hali ya kuondoa taka kwenye maeneo muhimu kama masoko, mitaa yenye watu wengi, kuhakikisha mitaa imefagiliwa na kuzungukiwa kwa maana ya kuhakiki zoezi la siku nzima. Manispaa kwa kujituma sana tunaondoa taka kwa asilimia 80.

003

Mfanyakazi wa manispaa ya Moshi akifagia barabara.

 • Vile vile tunalenga pia kwenye yale maeneo yenye takataka chache ambapo taka chache zinakuwa chukizo kwenye macho yetu pamoja na watalii.  Pia tunashirikisha umma kwa kupitia vipeperushi, mikutano, radio na kuwatumia Mabwana Afya kikamilifu.  Aidha, vikundi vya usafi vilivyoingia mkataba na Halmashauri; vikundi jamii vinaondoa taka kwenye majumba ya watu na kuweka kwenye maghuba.
 • Kwa hivi sasa tumeweza kuhamasisha Kata na Mitaa, pamoja na vikundi vya jamii kuingia majumbani, kukusanya ada za taka za Tshs. 1000/= kwa kaya kila mwezi; taasisi, maduka n.k. Fedha hizi zinakusanywa kwa stakabadhi za Halmashauri ya Manispaa na zinatumika katika ununuzi wa mafuta, kulipa motisha wafanyakazi, kutengeneza magari yanayoharibika n.k.
 • Utaratibu huu ni mzuri sana ; unawapa uwezo ngazi za chini kujiletea maendeleo yao kupitia usafi na vile vile kukuza ajira kwa vikundi jamii.
 • Pia Mji Dada wa Delray Beach huko Marekani wapo mbioni kuja kuimarisha vikundi kazi kwa kupitia mradi wao wanaotufadhili Manispaa ya Moshi.

oo4

Picha hii inaonyesha mojawapo ya maghuba yalitolewa na mradi wa kuboresha Manispaa ya Moshi uliofadhiliwa na mji rafiki wa Delray Beach uliopo Florida Marekani.

 • Kutokana na mfumo huu, Mji wa Moshi umeendelea kuboresha suala la usafi hadi ngazi ya chini ya mtaa na hadi kwenye kaya.  Kazi ya Manispaa ni kusimamia mfumo huu, ili usikwame na kuendelea  kudumisha utamaduni wa usafi wa mazingira.
 • Taasisi pia zinajishughulisha kikamilifu katika kupendezesha mizunguko (roundabouts) kumi, kwa kuotesha ukoka na maua na kuzishughulikia kila siku.

0006

Pichani ni mzunguko wa barabara ya Moshi-Arusha unaotunza na wadau wadau wa usafi wa Mazingira Tanzania Breweries Ltd.

 • Taasisi hizi ni Tanzania Breweries, Serengeti Breweries, Mamlaka ya majisafi na taka (MUWSA), Bonite Bottlers, Laliga Club, Tanzania Discovery Heritage na Mawenzi Sports Club.  Pia halmashauri inaendelea kutangaza zabuni kila mwaka za kuwataka wawekezaji waombe maeneo ya wazi na kuyaendeleza kufuatana na matakwa na mipango yake.  Aidha wanatumia maeneo haya kwa kuweka matangazo machache sana ya taasisi zao

2.1  Gharama za usafi:

Gharama za usafi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ni kubwa sana na zinavuka zaidi ya Tshs. 250m.kwa mwaka.  Sheria yetu ndogo ya mwaka 2006 imebainisha viwango vinavyokusanywa kwa watu kwa mwaka kama vifuatavyo:-

 • Hotels 260,000/=      Kwa mwaka
 • Mgahawa 80,000/=    Kwa mwaka
 • Duka la jumla 60,000/=  Kwa mwaka
 • Viwanda vikubwa/Taasisi 780,000/= Kwa mwaka
 • Viwanda vidogo 260,000/= Kwa mwaka
 • Biashara nyinginezo 36,000/= kwa mwaka
 •  Nyumba za kuishi 12,000/= kwa mwaka
 • Masoko /bus stand   15,000/= kwa  tripu
 • Ada ya ushuru wa dampo 5,000/= kwa tripu

Hivyo ada hizi zikikusanywa kwa asilimia 90, Manispaa inaweza kujipatia Tshs 180,000,000/=. Kwa mwaka. Halmashauri kupitia vyanzo vingine vya mapato ya ndani inachangia kiasi kinachopungua.

New Picture (2)

Mojawapo ya vifaa vinavyotumika(wheel Loader) katika Land fill (Dampo la kisasa) kwa kazi ya kusuma na kusambaza taka.

 

RASILIMALI ZILIZOTUMIKA KWA MIAKA MITATU

Usafi wa mazingira ni kipaumbele namba moja katika Halmashauri ya Manispaa Moshi kwa kuwa Halmashauri ina amini afya za wakazi wake ni muhimu kuliko masuala mengine yote (Kinga ni Bora kuliko Tiba) hivyo kwa muda wa miaka mitatu (2011-2013) imetumia kiasi cha zaidi ya Tshs. 1.2 billioni kutokana na vyanzo mbali mbali vifuatavyo

Chanzo cha fedha 2011 2012 2013
Vyanzo vya ndani 256,000,000.00 200,500,000.00 374, 513,000.00
Ruzuku toka Serikali kuu 25,500,000.00 12,000,000.00 5,000,000.00
Wafadhili wa ndani na nje 95,487,000.00 185,000,000.00  51,000,000.00
Jumla 376,987,000.00 397,500,000.00 430,513,000.00

 MATOKEO NA MAFANIKIO:

 1. Mji wa Moshi umepata mafanikio makubwa katika suala la usafi wa mazingira.  Halmashauri ya Manispaa imeweza kuwa ya kwanza katika mashindano ya kitaifa ya usafi wa mazingira kati ya Manispaa 17 nchini ambapo  siku ya Mazingira duniani kila mwaka, mwezi Juni, tarehe 5 tumekuwa tukipata tuzo za ushindi kwa miaka 7 hadi 2013 mfululizo. Ni kutokana na rekodi hiyo Shirika la Makazi Duniani UN-Habitat ilitutambua pamoja na nchi tatu nyingine za Afrika ambazo ni Lusaka – Zambia, Salaga  Ghana, Bamako – Mali na kuweza kuingizwa kwenye machapisho ya jarida la Kimataifa kuhusu udhibiti bora wa taka ngumu duniani ambalo lilizinduliwa Rio De Janeiro Aprili 2010 na uongozi wa Manispaa ulihudhuria.
 2.  Tumeweza kuwapokea wageni mbalimbali kutoka Halmashauri 13 za Kenya na walijifunza sheria yetu ndogo ya usafi wa mazingira pamoja na kubadilishana uzoefu na tuliweza kuwapa nakala za sheria walivyorudi kwao.Vile vile tumepokea zaidi ya Halmashauri 43 za hapa nchini.
 3. Tumefanikiwa kushusha madaraka ya kuratibu masuala ya usafi wa mazingira katika ngazi za kata (decentralization) kutoka ofisi kuu na watumishi wa ofisi za kata pamoja na majukumu mengine wamefanikiwa kukusanya fedha za ada za taka kutoka kwa wafanyabiashara, wananchi na taasisi nyinginezo   kwa taratibu zote za mapato na matumizi ya fedha za umma, pia kata huandika taarifa ya mapato na matumizi kila kipindi cha miezi mitatu na kuwasilishwa kwa mkurugenzi pamoja na vikao vya kamati husika.
 4. Tumefanikiwa kujenga utamaduni kwa wakazi wa Manispaa katika kuthamini usafi wa mazingira na jamii imeona umuhimu wa uchangiaji wa huduma za usafi na utunzaji wa mazingira, upandaji na utunzaji miti na pia halmashauri kuweza kusimamia sheria ndogo za usafi wa mazingira.

Ulipaji wa wakazi willingness to pay umefikia asilimia asilimia 95 kwa eneo la kati ya Mji, maeneo mengineyo yaliyopimwa asilimia 70 na maeneo ya pembezoni mwa mji asilimia 40

 1. r
  1. miti na utunzaji wa mazingira ni kipaumbele katika Manispaa ya Moshi.Picha hii inaonyesha utunzaji na upandaji katika Shule ya Msingi Mwereni.
  2. 2.    Manispaa ikishirikiana na Mamlaka ya Maji safi na Taka Mjini (MUWSA) tumeweza kutakasa maji ya bomba na  kupata kiwango cha ubora cha  TBS  na hivyo kuwezesha wakazi kuepuka magonjwa ya kuhara, kuhara damu na haswa kipindupindu. Hii inawezesha watu kupunguza gharama za hospitali na kuweza kuendelea na shughuli zao za maendeleo.(takwimu za magonjwa kabla na baada zionyeshwe)

  Takwimu za magonjwa 2010 

    Umri Chini ya miaka 5 Umri zaidi ya miaka 5
  Ugonjwa Idadi ya wagojwa Idadi ya vifo Idadi ya wagojwa Idadi ya vifo
  Kipindupindu

  0

  0

  0

  0

  Kuhara

  138

  12

  264

  17

  Typhoid

  148

  4

  253

  18

  Kuhara damu

  22

  0

  41

  0

  Takwimu za magonjwa 2013

 2. 0006
 3. Mzunguko wa barabara ya Taifa(Round about) ya YMCA inayotunzwa na mojawapo wa wadau wa usafi na mazingira Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Mjini(MUWSA) 

  CHANGAMOTO:

  1. Tatizo la wamachinga wanao zurura kila mahali mjini moshi kufanya biashara licha yakujengewa eneo.
  2. Ukosefu wa vitendea kazi vya kutosha
  3. Uchakavu wa magari na upungufu wa mitambo ya kuendesha dampo la kisasa.
  4. Watumishi wa usafishaji mji kuwa wachache, hii inatokana na sera ya serikali kusitisha ajira kwa kada hii.
  5. Ufinyu wa bajeti ya usafishaji mji
  6. Uchakavu wa miundo mbinu ya kusafirishia maji taka(mtandao wa mabomba ya maji taka) unaosababisha baadhi ya maeneo kuziba mara kwa mara.

   

  MIKAKATI YA KUPAMBANA NA CHANGAMOTO

   

  I.        Kuwa na mipango madhubuti katika kuimarisha shughuli za usafi wa mazingira kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali.

   

  II.        Kuendelea kusimamia sheria za kulinda afya na kutunza mazingira.

   

  III.        Kutembelea na kujifunza kwenye miji mingine misafi katika Afrika.

   

  IV.        Kununua gari 1 ya kubeba maghuba ya taka (skip master)

   

  V.        Kununua magari mengine manne (4) ya taka yenye uwezo wa kushindilia taka.

   

  1.                  VI.        Kuelimisha wakazi jinsi ya kutenganisha taka ngumu kuanzia kwenye Kaya (Separation at source) kwa ajili ya kuongeza kiasi na ubora wa taka rejea zinazotumika kama mali ghafi viwandani.

   

  1.                VII.        Kuboresha dampo la kisasa linalotumika ikiwa ni pamoja na kujenga mtambo wa kufua gesi (biogas plant).Hii inatarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano wa mji dada wa Tuebingen Ujerumani.

  SIRI YA MAFANIKIO

  1. Suala la usafi katika Manispaa ya Moshi limeshushwa Katika ngazi ya kata (decentralization) na kusimamia na kamati ya maendeleo ya kata na watumishi katika kata wanawajibika kukusanya fedha za ada taka kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi na kuzitumia fedha hizo kwa kufuata taratibu za matumizi ya fedha za umma.Fedha hizi hutumika kuwalipa wafagizi,kuweka gari mafuta kwa ajili ya magari yakusafirisha taka ngumu kwenda kwenye dampo. Ofisi kuu imebakia na jukumu la kusimamia utekelezaji na kutoa ushauri na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.Hali hii imesababisha wananchi kuchangia ada kwani wanapata huduma kwa wakati na vile vile wanapata taarifa ya mapato na matumizi ya ada za taka kupitia kwa waakilishi wao na mikutano ya hadhara ya kwenye mitaa.
  2.  Manispaa ya Moshi ni Mji uliopangwa vizuri kuanzia enzi za ukoloni na kuna makazi machache yasiyopangwa kama sehemu ya maeneo ya Mji mpya na Njoro. Hata hivyo, Manispaa imekuwa na mradi mkubwa ambao wakazi wanashirikishwa kupanga maeneo yao na kutengeneza mifereji wa maji ya mvua.Vile vile Manispaa ya Moshi imeweza kuzuia  ujenzi  holela na hali hii imesababisha vichochoro vyote katika ya mji vipo wazi,vinapitika na vinafanyiwa usafi .

  009

Picha hii inaonyesha mojawapo ya vichochoro katika ya mji (kichochoro cha Del Chez).Wakazi wa Manispaa ya Moshi wanawajibika kusafisha na kutunza mbele na nyuma ya maeneo yao wanaoishi au kufanya biashara kila siku.

1. Aidha, utekelezaji wa miradi mbalimbali kama ujenzi wa barabara mpya, ukarabati wa barabara, ujenzi wa mifereji vinatekelezwa kwa ufanisi mkubwa  na kuchangia katika kuweka mazingira safi. . Halamshauri ya Manispaa Moshi ina mtandao wa barabara wenye urefu wa km 288.039. Kati ya barabara hizo km 76.643 ni barabara za Lami, km. 79.312 ni barabara za changarawe na km 132.084 ni barabara za udongo.Matengezo na ukarabati wa barabara tunatumia mfuko wa barabara na mapato ya ndani.Manispaa ya Moshi in sera yake ya kujenga Km 1 ya barabara za lami kwa kutumia mapato yake ya ndani kwa kila mwaka wa fedha. Barabara hizo zinapitika majira yote ya mwaka.

007

 1. Ushirikishwaji wa wadau wa usafi wa mazingira kama vile Wakala wa Barabara ,Chuo cha Polisi Moshi,mkuu wa gereza la Karanga katika  ufyekaji majani kando ya barabara wakati wa masika majani yanapokota kwa wingi hali hii husaidia kuendelea kuiweka Manispaa ya Moshi katika hali ya usafi na kupendeza wakati wote.

 1. Mji wa Moshi unapata maji safi na salama kwa asilimia 98 na pia kuna mfumo wa maji taka.  Maji safi ya Moshi yana nembo ya ‘Bureau of Standards’ na hivyo kuchangia sana katika usafi wa mazingira.  Mfumo wa maji taka umetandazwa kwa asilimia 44 na kuweza kuzidi viwango vya Kenya na Uganda yaani East Africa. Maji taka yote yanaelekezwa kwenye mabwawa ya kutakasia ‘oxidation ponds’ yaliyojengwa chini ya mradi wa kuboresha miundo mbinu katika miji (USRP) kwa gharama ya Tshs. 4.8 bilioni na yalikamilika novemba1999.

0002

Baadhi ya watumishi wakionekana kuwapa maelezo wadau waliokuja Manispaa ya Moshi  kujifunza masuala ya mfumo wa utakasaji maji taka  katika eneo la mabwawa ya maji taka yaliyopo  eneo la mabogini

 

 1. Manispaa ya Moshi ina Miji Dada ya Komaki Japan, Halmstad Sweden, Delray Beach Marekani, na Tuebingen Germany.  Tumeweza kushirikiana na miji hii katika masuala ya usafi wa mazingira, elimu na demokrasia.  Tumefaidika sana na safari za kutembeleana na kuona kwa kujifunza usafi wa mazingira uliovuka mipaka yote, masuala ya uzungushaji taka (waste recycling) na kuweza kufua umeme.Vile vile tumeweza kupata misaada ya gari la kuzoa taka na maghuba 12 ya kuwekea taka

Idadi ya wadau waliotembelea miji dada na kipindi

Na. Jina la Mji/Jiji Mwaka Idadi Msaada uliopatikana
1. Komaki – Japan 2008 6 Gari la kuzoa taka ngumu (ISUZU FUSO)
2. Delray Beach Marekani 2011 & 2013 6 Maghuba (skip buckets) 12 ya kuhifadhi ngumu
3. Tuebingen Germany 2011 & 2013 5 Utafiti kwa ajili ya mradi wa ‘Bio gas’

 l

Mojawapo ya gari la kuzoa na kushindilia taka ambalo Manispaa ya Moshi imepata msaada kutokana na ushirikiano uliopo na Mji wa Komaki-Japan.

10. Pia tumefanikiwa kujenga utamaduni kwa wakazi wa Manispaa katika kuthamini usafi wa mazingira na uoteshaji miti.

11. Halmashauri  imeunda Vikundi maalum vya kutimamia usafi wa mazingira katika kata za Manispaa ya Moshi kwa lengo la kusimamia kwa karibu usafi wa mazingira kwenye kata.  Wajumbe wa vikundi wanatoka kwenye kila Mitaa ya kata husika. Wajumbe hao wanatakiwa kuwa na sifa zilinazotakiwa na Halmashauri na wanatakiwa kuomba nafasi hizi na kujadiliwa na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC) ambapo ukubwa wa kikundi (idadi ya wana kikundi) unazingatia ukubwa wa kata husika.

Vikundi vinawajika na kusimamiwa na kata na vinfanya kazi kwa mujibu wa sheria ndogo za Halmnashauri ya Manispaa Moshi na jukumu namba moja ni kudhibiti uchafuzi wa mazingira.  Aidha wanatoa faini kwa mujibu wa sheria ndogo ya usafi  mazingira kiwango cha faini ni kati ya 10,000/= hadi 50,000/= kulingana na uzito wa kosa.

12. Pia Halmashauri inashirikiana na Polisi Jamii  kudhibiti uharibifu wa uchafuzi wa mazingira nyakati za jioni kuanzia saa 12.00. Wanakamata mifugo inayozurura, ukataji miti bila kibali pamoja na wananchi wanaotupa taka maeneo yasiyoruhusiwa nyakati za jioni na usiku .Polisi jamii kwa kiasi kikubwa wanasaidia kupunguza uanzishwaji wa majalala holela yasiyo rasmi kwenye maeneo ya makazi, biashara na maeneo ya wazi.

13. Vile vile Halmashauri inatumia  vikundi vya mazingira RAKAS na BORESHA ambavyo vinafanya kazi ya kudhibiti wachafuzi wa mazingira katika maeneo ya katika ya mji hasa katika kata za Bondeni,Kiusa na Mawenzi.Vikundi hizi vinatoza wachafuzi wa Mazingira faini isiyozidi Ths 50,000/= kwa mujibu wa Sheria ndogo za Halmashauri ya Manispaa na kila mwezi wanalipa Tshs. 400,000/= (laki nne) kutokana na sehemu ya mapato ya faini wanazotoza na wao wenyewe kumudu gharama za kujiendesha.

14. Manispaa imeweka matangazo ya mabango yanayokatakaza kutupa taka ovyo katika barabara za  kuingia na kutoa Manispaa ya Moshi ,katikati ya mji na katika kituo kikuu cha mabasi Moshi.Vile vile matangazo yanayotolewa na kwa kutumia kipaza sauti katika Kituo Kikuu cha Mabasi kuwawatahadharisha wasafiri kutii sheria ndogo ya usafi wa mazingira na kuacha kutupa taka ovyo kwa lengo la kuepuka usumbufu na faini zisizo za lazima.

15. Kwa kuwa usafi ni kipaumbele namba moja katika Manispaa ya Moshi kila kiongozi kwa nafasi yake analitambua hili kuanzia kwenye Timu ya Menejimenti na Viongozi wa kuchaguliwa kama Wah. Madiwani.  Katika vikao vya kamati za Maendeleo za Kata (WDC) suala la usafi ni agenda ya kudumu ambapo taarifa za utekelezaji na changamoto zinapatiwa ufumbuzi katika ngazi ya kata, zile ambazo zinashindikana katika kata zinawasilishwa Halmashauri kwa utatuzi.

16. Vyoo vya umma vimejengwa na Halmashauri katika maeneo ya umma kwa kutumia fedha za halmashauri.  Pia vyoo vitatu vilivyojengwa kwa utaratibu wa uwekezaji ambapo mwekezaji amejenga kwa gharama zake na baada ya kukamilika anapewa mkataba wake muda maalum wa kuendesha choo alichojenga kwa lengo la kurejesha gharama zake za ujenzi.   Baada ya kurejesha gharama choo kinabaki kuwa mali ya halmashauri.Uendeshaji wa vyoo vya umma katika Halmashauri unafanywa na Mawakala wanaopatikana kupitia zabuni ambao huwajibika kutoa huduma na pia kuingizia kipato Halmashauri.  Mapato ya vyoo yamekuwa yakiongezeka na pia kiwango cha usafi kuimarika.  Kwa mwaka wa fedha 2011/2012 zilipatikana Tshs. 19.6mil. mwaka 2012/2013 Tshs. 25.4mil. na 2013/2014mil. tunatarajia kupata 29.6 ifikapo Juni 2014.

17. Mashindano ya usafi wa mazingira yanafanyika kila mwaka kwa lengo la kuchochea kata kuongeza bidii katika usafi.

Vigezo vinavyotumika katika mashindano ya kata vimeandaliwa kutokana na vigezo vya mashindano ya kitaifa  kwa lengo la kufanya matayarisho ya mashindano ya kitaifa na kuweka mazingira mazuri ya kufanya kushinda.

Timu ya majaji watano (5) inahusisha watalaam wa Idara ya Afya na Idara ya Usafi wa Mazingira pamoja na watalaam wa nje toka Sektretariet ya Mkoa ambao ndio wanaoendesha mashindano hayo katika kata 21 za Manispaa ya Moshi. Kata tatu bora zinapewa tuzo ya fedha taslimu pamoja na vyeti.  Kata ya kwanza Tshs. 300,000/= ya pili Tshs. 200,000/= na tatu Tshs. 100,000/=.  Vyeti hutolewa wakati wa maadhimisho ya siku ya Serikali za Mitaa/Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Comments are closed.